Utume wa Mama Hannah (UMH) ni vuguvugu la kitume la Kanisa Katoliki linayofanya kazi zake chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia Idara ya Katekesi. UMH umejikita katika kuhamasisha, kuimarisha, na kusaidia wito wa Makatekista, ambao ni mhimili na msingi katika utume wa Kanisa, hasa katika kazi ya kurithisha Imani na kueneza Injili ya Kristo kwa vizazi vilivyopo, na kwa vizazi vijavyo.
Kanisa Katoliki, tangu mwanzo, limeutambua wito wa Makatekista kuwa ni kiini cha maisha ya imani ya waamini wake. Makatekista wamekuwa wasaidizi muhimu wa Maaskofu na Mapadre katika kufundisha, kusimamia makundi ya waamini, na kuandaa waamini kupokea Sakramenti Takatifu. Kwa sehemu kubwa, karibu kila Mkristo Mkatoliki, awe Askofu, Padre, Mtawa, au mwamini wa kawaida, amepokea mafundisho na malezi ya kwanza ya imani kupitia huduma ya Katekista. Kwa kupitia Makatekista waamini wengi wamepata kufundishwa, kubatizwa, kuandaliwa kwa Komunio ya Kwanza, Kipaimara, Ndoa, na hata wito wa Daraja Takatifu.
Pamoja na nafasi yao adhimu katika Kanisa, hali halisi ya Makatekista wengi haioneshi kutambuliwa ipasavyo. Wengi wanatoa huduma kwa kujitolea, wakiwa na changamoto za kiuchumi, kijamii, kimazingira, na kielimu, jambo linalopelekea kupungua kwa ubora wa malezi ya kiimani na kulegalega kwa misingi ya mafundisho sahihi ya Kanisa. Katika baadhi ya maeneo, mafundisho ya imani yanatolewa kwa kiwango cha chini, hali inayosababisha waamini wengi kushindwa kudumu katika Imani Katoliki na wengine hata kupotea katika mapokeo ya imani nyingine.
Kutokana na changamoto hizo, Utume wa Mama Hannahh umebainisha haja ya kufanya jitihada za makusudi kukuza na kuimarisha wito wa Makatekista kwa kuwasaidia kielimu, kiuchumi, kijamii, na kiroho. UMH unalenga kuwa daraja kati ya walengwa na wadau mbalimbali wa Kanisa, ukiunganisha nguvu za Maaskofu, Maparoko, Wakurugenzi wa Katekesi Majimboni, Wakuu wa Vyuo vya Katekesi, Mashirika ya Kidini, na waamini wote wenye nia njema, ili kuhakikisha kuwa wito huu wa Ukatekista unathaminiwa, unalelewa, na unastawi.
Kupitia elimu, hamasa, maombi, sala, kufunga, na michango ya kifedha na vifaa, UMH ni chombo cha matumaini kwa Makatekista waliopo na wale wanaojiandaa kwa huduma. Utume utaunda na kudumisha mfumo wa wachangiaji wa kudumu, wa mara kwa mara, na wa papo kwa papo ili kufanikisha upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika malezi na maendeleo ya Makatekista.
Kwa ujumla, Utume wa Mama Hannah (UMH) ni alama ya upendo, huruma, na ukarimu wa kiroho kwa Kanisa. Ni mwitikio wa imani kwa wito wa Kristo aliyesema: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache” (Mathayo 9:37). Ni mwaliko wa kushiriki kikamilifu katika kuandaa, kulea, na kuwawezesha Makatekista kuwa mashahidi hodari wa Injili, ili Kanisa liendelee kukua katika imani, matumaini, na upendo kwa wokovu wa ulimwengu wote.